Serikali imeliambia Bunge kuwa tayari baadhi ya makampuni makubwa ya madini yameanza kulipa fidia kutokana na kubainika kuwa walikwepa kodi na tozo mbalimbali na kuwa zoezi hilo litahusu kampuni zote za madini.
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesema hayo bungeni mkoani Dodoma wakati wa kuhitimishwa kwa bajeti ya Wizara ya madini kwa mwaka wa fedha 2018/19 na kusema kiasi cha fedha kinacholipwa na kampuni hizo kama fidia kwa sasa ni siri ya serikali.
Naye Mwanasheria mkuu wa serikali Dokta Adelardus Kilangi amesema sheria mpya za madini zilizotungwa hivi karibuni zimelenga kufanya rasilimali za madini kulinufaisha taifa na hazina madhara kwa taifa kwa kuwa zimezingatia sheria mama za madini duniani.
Baadhi ya wabunge wamesema ipo haja ya wizara hiyo ya madini kuzidi kuziangalia taasisi zilizo chini yake ziweze kutimiza wajibu wao ipasavyo na kulifanya taifa linufaike na sekta ya madini.