Back to top

Tanesco yatakiwa kubadilika katika utoaji huduma.

09 September 2018
Share

Shirika la umeme nchini– TANESCO mkoani Mtwara limetakiwa kubadilika kwa kuwafuata kwenye maeneo ya ujenzi wawekezaji wanaojenga viwanda, ili kuwapatia huduma za umeme, badala ya kusubiri mwekezaji kuja kuomba ofisini, utaratibu alioelezwa kuwa umepitwa na wakati.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa alipotembelea mradi wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kubangua korosho cha Yalin Cashenut Company Limited toka china eneo la Mayanga Mtwara vijijini kilichopanga kuanza ubanguaji mwezi wa 11 mwaka huu, katika ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa viwanda na kukuta shughuli za kuunganisha vyuma kiwandani hapo zikifanywa kwa kutumia jenereta, badala ya umeme wa TANESCO.

Mapema, akitoa taarifa ya uwekezaji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara Omari Kipanga amesema katika kuitikia mpango wa serikali wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda, halmashauri hiyo imetenga eneo hilo la mayanga, lenye ukubwa wa ekari 4,600 kuwa eneo maalumu la viwanda.

Mapema kwenye ziara hiyo Mkuu wa Mkoa Gelasius Byakanwa alitembelea kiwanda cha kusaga unga wa mihogo kijiji cha Mtendachi na kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti kijiji Mnyija kata ya Mpapura na kuelezwa viwanda hivyo vinatumie mafuta ya Deseil katika uzalishaji, kwa kuwa havijapatiwa umeme.