Back to top

Wanunuzi wa korosho Mtwara watahadharishwa kuwaepuka madalali.

13 October 2018
Share

Serikali ya mkoa wa Mtwara imetoa hadhari kwa wanunuzi wa zao la Korosho kutoka India, China, Vietinamu na Ghana walioko mkoani humo kununua Korosho, wawaepuke madalali katika ununuzi wa zao hilo, badala yake waitumie Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bodi ya Korosho, ama ofisi za wakuu wawilaya ili kujiweka salama katika biashara hiyo.

Mkuu wa Mkoa huo Bwana Gelasius Byakanwa ametoa hadhari hiyo wakati akitambulisha rasmi ufunguzi wa msimu wa Korosho kwa mwaka 2018/2019 ambao minada itaanza rasmi Octoba 22 mwaka huu.

Amesema ni vema wafanyabiashara hao wakatumia ofisi hizo kufanikisha ununuzi wa Korosho, badala ya kuwatumia madalali  ambao baadhi yao siyo waaminifu na wanaweza kuwaingiza kwenye matatizo.

Hata hivyo, amesema mkoa umejipanga vema katika msimu huu na tayari vifungashio vya Korosho yakiwemo magunia vimewasili mkoani humo na kusisitiza kuwa hali ya ulinzi na usalama kwa wageni wanaoingia Mtwara ni salama.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wamewaomba wakulima wahakikishe kuwa Korosho watakazopeleka kwenye vyama hivyo baada ya minada kufunguliwa zinakuwa safi na zenye viwango vinavyokubalika kimataifa, ili kuendelea kulinda soko la ndani.