Back to top

Mahakama ya Kisutu yamfutia dhamana Mbowe na Matiko.

23 November 2018
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mhe.Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini Mhe.Esther Matiko kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Akitoa uamuzi huo wa kuwafutia dhamana viongozi hao wa -CHADEMA-Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard  Mashauri amesema sababu za kutofika mahakamani zilizotolewa na mdhamini wa Mheshimiwa Mbowe kuwa tarehe Nane mwezi huu mshitakiwa huyo aliugua ghafla na kupelekwa nje ya nchi akiwa mahututi, wakili wake  kueleza kuwa alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu ni za uongo sababu zinakinzana na taarifa alizotoa mshitakiwa mwenyewe.

Kuhusu Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe.Esther Matiko, hakimu Mashauri amesema Tanzania inaongozwa kwa sheria na sheria inamtaka mshitakiwa yo yote pamoja na cheo chake alichonacho bado yupo sawa na watu wengine wanyonge hivyo bado anatakiwa kutimiza amri za mahakama, hivyo sababu alizotoa Mhe. Matiko kuwa alihudhuria ziara ya kibunge nchini Burundi si za msingi na hazikidhi matakwa ya kutofika mahakamani.

Kutokana na uamuzi wa mahakama, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala umewasilisha hati ya dharura sana Mahakama Kuu ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai washtakiwa hao walishafika mahakamani tarehe 12 na 23 hivyo haiwezekani kumfutia dhamana mshitakiwa aliyefika mahakamani mara mbili mwenyewe na kutoa maelezo ya sababu kutofika mahakamani.

Kutokana na upande wa utetezi kukata rufaa Mahakama Kuu kwa kuwasilisha hati ya dharura, Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard  Mashauri amesema kesi hiyo itatajwa tarehe 6 mwezi ujao kwa ajili ya kutajwa wakati ikisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu maombi la upande wa utetezi na washtakiwa wamerudishwa rumande.