Basi lenye uwezo wa kubeba abiria 60 linalofanya safari zake kuanzia Arusha kwenda kiteto mkoani Manyara limekamatwa na polisi likiwa limebeba abiria zaidi ya 100 kitendo kinachodhihirisha jinsi baadhi ya madereva na makondakta wanavyochezea maisha ya watu na kukiuka sharia.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha Bw Joseph Bukombe amesema kukamatwa kwa basi hilo lenye namba za usajili T 945 AAU la kampuni ya Kimotco hayo ni matokeo ya operesheni ya kufuatilia mabasi yote yanayokwenda mikoani inayoanywa na kikosi maalumu cha polisi inayolenga kukomesha ukiukwaji wa sharia unaoendelea kufanywa na baadhi ya madereva na pia baadhi ya askari wasio waaminifu.
Wakati kondakta wa basi akidai kuwa waliokuwa wamezidi kwenye basi ni wanafunzi na walimu na baadhi ya abiria wakidai kuwa wanalazimika kupanda magari yaliyojaa kutokana na uhaba wa mabasi , mmiliki wa basi hilo Bw Benedikti Mberesero amesema yeye hajawatuma dereva na kondakta wake kuvunja sheria na kwamba kitendo walichofanya hakikubaliki na yeye hakiungi mkono.