Back to top

Serikali yaagiza kufunguliwa dawati maalum la malalamiko ya likizo.

01 August 2019
Share

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza kufunguliwa kwa madawati maalumu ya kuwasilisha malalamiko kwa waajiri ambao hawatoi likizo ya uzazi kwa watumishi wao wa kike wanapojifungua ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ya kazi ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2015.
 
 
Mhe.Mwalimu ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akizindua wiki ya unyonyeshaji iliyobeba kauli mbiu wawezeshe wazazi, kufanikisha unyonyaji ambapo amesema kuna waajiri wamekuwa ni sugu katika kutoa likizo ya uzazi kwa watumishi hao ambapo amewataka wafanyakazi watakaonyimwa haki hiyo ya msingi kutoa taarifa kwa maafisa kazi pamoja na kuwatengea saa mbili za unyonyeshaji kwa siku za kazi.
 
Aidha waziri Mwalimu ameagiza ofisi za umma kuwepo kwa vyumba maalum vya faragha vya kuwawezesha kinamama kunyonyesha watoto wao huku akidai kuwa mtoto asiponyonyeshwa maziwa ya mama atakumbwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo pumu, kipindupindu na kuathiri ukuaji wake kwa kupata udumavu.
 
Kwa upande wake, mwakilishi mkazi wa umoja wa mataifa UN Bw.James Gitau amesema UN itaendelea kuiunga mkono serikali kwenye miradi inayohusiasana na uhamasishaji unyonyeshaji watoto.