Back to top

Mbowe ashambuliwa na wasiojulikana avunjwa mguu jijini Dodoma.

09 June 2020
Share

Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amejeruhiwa baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo jijini Dodoma.

Taarifa za awali kutoka CHADEMA zinaeleza kwamba tukio hilo lilitokea wakati kiongozi huyo akirejea nyumbani kwake.

Mhe.Mbowe amelazwa katika hospitali ya DCMCT Ntyuka mkoani Dodoma anapoendelea kupatiwa matibabu huku mguu wake mmoja ukiwa umevunjika.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, amezungumzia sakata hili na kusema Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, amevamiwa na watu watatu waliomkanyaga na kumvunja mguu wake wa kulia.

"Zipo taarifa kwamba Mhe.Mbowe amevamiwa na watu watatu, wakamkanyaga kanyaga na kumvunja mguu wake wa kulia, lakini tunafuatilia tutatoa taarifa kamili baadaye na yuko Hospitali ya Ntyuka wodi namba 4" amesema Kamanda Muroto.

Naye Mhe.Ester Bulaya ambaye ni Mnadhimu wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema kwa sasa wanafanya utaratibu ili kiongozi huyo aweze kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa Matibabu zaidi.

Amesema viongozi wa Chama hicho walipo pata taarifa ya kushambuliwa kwa kiongozi huyo walifika na kutoa msaada wa kuweza kumfikisha hospitali, ambapo mpaka sasa wabunge mbalimbali wapo eneo hilo kuona taratibu zingine zinavyoendelea.

Kwa upande wake Mbunge wa Iringa mjini (CHADEMA), Mhe.Peter Msigwa amesema kwa maelezo ya Mhe.Freeman Mbowe watu hao waliomvamia walikuwa watatu na walivalia makoti meusi, huku wakimwambia "Unaisumbua sana Serikali, tunataka tukuonyeshe kwamba serikali ipo, tuone na kampeni yako utafanyaje, kwa hiyo wakasema sisi hatuna mpango wa kukuuwa ila tunataka tukuvunje ushindwe kufanya kampeni", aliyaeleza Mbowe maneno hayo mbele ya Mhe.Msigwa.

Spika wa Bunge Mhe.Job Nduga na Naibu Spika Mhe.Tulia Ackson ni moja ya viongozi waliofika kwenye hospitali ya DCMCT Ntyuka mkoani Dodoma kuona hali ya Mhe.Freeman Mbowe ilivyo baada ya kushambuliwa na watu watatu wasiojulikana na kumvunja mguu.