Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wenye tabia ya kuwaficha watoto Wenye Ulemavu kuacha mtindo huo badala yake wahakikishe wanawapa fursa ya kupata elimu.
Ametoa kauli hiyo alipofuturu na watoto wenye mahitaji maalum wa kituo cha Buigiri, Wilayani Chamwino ambacho kinamilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika.
Amesema ili kuhakikisha watoto hao wanapata Elimu, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia mahitaji mbalimbali kwa ajili kujifunza na kufundishia.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamisi amesema kuwa tukio hilo ni ishara ya upendo wa viongozi wakuu wa Serikali kwa kundi la watu wenye mahitaji maalum.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dkt.Dickson Chilongani ameshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa uamuzi wake wa kuamua kula futari na watoto wenye mahitaji maalum wa kituo cha Buigiri, Wilayani Chamwino.
Aidha Askofu Dkt.Chilongani amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa Kanisa hilo linaendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Sita katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kudumisha amani.