Back to top

Waziri Mkuu ataka kasi ujenzi barabara ya mzunguko Dodoma

04 September 2022
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango.
 
“Kazi inaendela vizuri, tunataka kazi ikamilike ikiwezekana hata kabla ya muda, Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi hii ili iwanufaishe Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia na inakamilika kwa viwango na wakati”
 
Amesema hayo leo (Jumapili, Septemba 04, 2022) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma. Mradi huo ni sehemu ya uendelezaji wa jiji hilo.
 
Pia, Waziri Mkuu amewataka Wahandisi Wasimamizi wa mradi huo wahakikishe wanasimamia kikamilifu wakandarasi ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa ujenzi wake.
 
Akizungumza na watanzania walioajiriwa katika mradi huo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wawe walinzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi na wahakikishe vifaa vinabaki salama “Pambaneni na wote wenye nia ya kuiba vifaa hivi, tunataka tupate barabara yenye viwango”
 
Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda amesema kuwa pamoja na mradi huo kusaidia kupunguza msongamano wa magari jiji la Dodoma pindi utakapokamilika, pia umesaidia kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 800.
 
“Mheshimiwa Waziri Mkuu utekelezaji wa mradi huu utawezesha kujengwa kwa vituo vya afya vinne katika mitaa ya Mahomanyika, Veyula, Nala na Ihumwa. Pia yatanunuliwa magari ya wagonjwa manne katika vituo hivyo”.
 
Aliongeza kuwa sehemu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Nala-Veyula-Mtumba hadi bandari kavu ya Ihumwa (Km 52.5) unaojengwa kwa muda wa miezi 39, utagharimu shilingi bilioni 100.

“Sehemu ya pili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Bandari kavu ya Ihumwa-Matumbulu hadi Nala (Km 60) unaojengwa kwa muda wa miezi 43, utagharimu shilingi bilioni 120.8 ”