Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda amesema Serikali itawaondoa kwenye ranchi zake, wawekezaji wote wasiofuga kisasa au kulipa kodi ya vitalu walivyokodishwa.
Nzunda ametoa kauli hiyo mara baada ya kufika na kukagua baadhi ya vitalu vilivyopo kwenye ranchi ya Mkata iliyopo Mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuzitembelea ranchi zilizopo chini ya Kampuni ya ranchi za Taifa (NARCO).
"Serikali haitaruhusu ufugaji huu wa kienyeji ndani ya ranchi zake kwa sababu tunataka kuwa na ranchi zinazofanana na ranchi na kwa maneno mengine tungependa kuona wapangaji wetu waliopo kwenye ranchi zetu zote nchini wanakuja na mpango wa kufuga kisasa na kwa kuzingatia mipango ya biashara waliyonayo na kama hamuwezi kuzingatia mipango hiyo tutaomba mtupishe ili tubaki na wale wenye nia ya kufuga kisasa" Amesisitiza Nzunda.
Nzunda ameongeza kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa hainufaiki na rasilimali ya mifugo iliyopo nchini kutokana na kutofuata njia za ufugaji wa kisasa hivyo dhamira ya Wizara yake kupitia Sekta ya Mifugo ni kuhakikisha inaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuhakikisha sekta ya Mifugo inatoa mchango wa kutosha kwa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Nzunda ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha wawekezaji wote waliokodishwa vitalu kwenye ranchi za Taifa wanalipa madeni ya kodi wanazodaiwa ambapo amesisitiza kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo wataondolewa.
"Wawekezaji wamelalamika hapa kuwa sababu ya kutolipa kodi hiyo ni ukubwa wa kodi kutoka shilingi 1,500 kwa ekari waliyokuwa wakilipa mwanzoni hadi 7,500 iliyoongezeka tangu mwaka 2018 hivyo niwaagize NARCO waende wakarekebishe hilo na wadaiwa wote walipe shilingi 3,500 kwa kila ekari waliyokuwa wamependekeza afu baada ya hapo tufanye tathmini kwa ambao hawatalipa ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo tuwaondoe" Ameongeza Nzunda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ranchi za Taifa (NARCO) Prof.Peter Msoffe mbali na kukiri kupokea maelekezo hayo, ameahidi kuyawasilisha kwenye Bodi ya kampuni hiyo ili waweze kufanya tathmini ya madeni ya kila mwekezaji kwa kiwango kilichoelekezwa ndipo waanze kulipa.
Mbali na kutembelea baadhi ya vitalu vilivyopo kwenye ranchi ya Mkata, Nzunda amefanya kikao na baadhi ya wawekezaji waliopo kwenye ranchi hiyo ambapo amewasisitiza kufanya shughuli zao kwa kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.