Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi, amesema uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua, licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia.
Ametoa kauli hiyo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na waandishi wa habari nchini, katika utaratibu aliojipangia wa kukutana nao kila mwisho wa mwezi.
Amesema pamoja na changamoto za kuwepo kwa Ugonjwa wa Uvico-19 na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukrane, uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua, hususani kupitia sekta ya utalii, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watalii wanaozuru nchini.
Dkt.Mwinyi amesema ukuaji huo wa uchumi pia umechangiwa na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, ambayo imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 6.7 katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Julai hadi Septemba, 2022 na Bodi ya Mapato Zanzibar na Shirika la Bandari pia yamekuwa katika kiwango bora cha kukusanya kodi.
Aidha, amesema Sekta ya Uwekezaji nayo imepata mafanikio makubwa, ambapo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar imefanikiwa kusajili miradi mia moja themanini na moja yenye thamani ya zaidi ya Dola Bilioni tatu, huku wastani wa wananchi elfu kumi na moja mia mbili themanini na tisa wanatarajiwa kupata ajira.