Back to top

WASANII KIZAZI KIPYA EPUKENI KUIGA KILA TAMADUNI

11 November 2022
Share

Makamu wa Rais Mhe.Dakta Philip Mpango, ametoa wito kwa Watanzania wote, hasa wasanii wa kizazi kipya, kuepuka kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili ya taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo alipokuwa akifungua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo, linalofanyika katika  Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo Mkoani Pwani.

Ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wana zingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa, pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania wakati wa utengenezaji wa maudhui ya kazi zao, ili kuepukana na uvunjifu wa maadili unaojitokeza.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kutoa kipaumbele katika kuendelea kukitangaza Kiswahili duniani.

Kwa Upande wake, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe.Mohamed Mchengerwa, amesema Wizara hiyo inalenga kuinua kiwango cha Tamasha la Sauti za Busara Zanzibar pamoja na Tamasha la Bagamoyo ili yaweze kufikia viwango vya kimataifa na kufanana na matamasha makubwa duniani.