Serikali imekemea vitendo unyanyasaji, na udhalilishaji wenye misingi ya umri, jinsia, rangi, kabila, ulemavu pamoja na dini katika maeneo ya kazi.
Makamu wa Rais Dakta Philip Mpango, amekemea hayo Jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2022, zinazoratibwa na chama cha waajiri Tanzania.
Amesema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu, na vinaathiri utendaji wa kazi siyo tu kwa waathirika, bali kwa viongozi na taasisi au mashirika wanayofanyia kazi.
Amesisitiza kuwa kila mfanyakazi ana haki ya kutendewa utu, kuthaminiwa na kuheshimika kazini na kuagiza, kuwekwa mifumo itakayowezesha wafanyakazi kutoa taarifa za kunyanyaswa au kuonewa bila kuhofia madhara yoyote, yanayoweza kujitokeza ikiwemo kupoteza ajira zao.