Back to top

AFARIKI DUNIA KISA DAU LA KUOGELEA.

19 August 2024
Share

Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Kelvin Gitonga (25) amefariki dunia kwa kuzama kwenye maji, katika Eneo Bunge la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga, wakati akijaribu kuogelea katika bwawa la Mamlaka ya Kitaifa ya Umwagiliaji ili kushinda dau la Ksh 300 siku ya Jumapili.

Tukio hilo lilitokea usiku na kuwashtua wakazi wa Maisha Kamili katika Mji wa Ngurubani na Kijiji cha Kamucege.

Kelvin Gitonga, mwogeleaji na mwendeshaji bodaboda maarufu huko Ngurubani, anadaiwa kuweka dau na rafiki yake kwamba angeweza kuogelea kutoka upande mmoja wa bwawa hadi mwingine.

Kulingana na mashahidi, alikuwa karibu kufika ufukweni alipozama kwa njia ya kusikitisha. Rafiki yake aliyekuwa ameweka dau hilo alitoweka muda mfupi baada ya tukio hilo.

Philip Njogu, mkazi wa eneo hilo, alionyesha kutokuamini habari hizo. "Tulikimbilia kwenye bwawa mara tu tuliposikia, lakini ni ngumu kuamini kwamba Kelvin amezama kwenye maji, alikuwa muogeleaji mzoefu."

Kinyua Warui, wa mtaa mwingine, alisema. "Kelvin alijiamini kuwa ataweza, na alikuwa karibu kufika ufukweni ilipotokea. Hii si mara ya kwanza yeye na marafiki zake kufanya dau kama hilo."

Wakazi wa Kamucege na Ngurubani, wameitaka Mamlaka ya Kitaifa ya Umwagiliaji kulijengea uzio bwawa hilo huku wakitaja kuwa kifo cha hicho ni cha pili katika eneo hilo.