Wakala ya Barabara (TANROADS) imefunga mizani inayohamishika (mobile weighbridge) ya kudhibiti uzito wa magari katika eneo la Tunduma kwa ajili ya kupima magari yanayotoka Tunduma kuelekea Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa malori yanayosubiri kwa muda mrefu kupima uzito katika mzani mmoja wa Mpemba unaotoa huduma mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Ufungaji wa Mizani hiyo ni utelelezaji wa maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Novemba 18, 2024 wakati alipokagua na kujionea msongamano wa malori katika eneo hilo ambalo lilitegemea mzani mmoja wa Mpemba.
Akizungumza baada ya kukamilisha zoezi hilo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga amesema juhudi hizo ni matokeo ya maelekezo yaliyotolewa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kurahisisha ufanyaji biashara kupitia huduma ya usafirishaji.
"Waziri Bashungwa alitoa maagizo ya kutafuta suluhisho la haraka, na kwa kushirikiana na TANROADS Mkoa wa Mbeya, tumefanikisha kupunguza msongamano mkubwa uliokuwa ukisababisha usumbufu kwa madereva hapa Tunduma," alisema Mhandisi Bishanga.