Back to top

Atakaye bainika kuhusika na moto soko la Kariakoo kuchukuliwa hatua.

11 July 2021
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ametoa siku 7 kwa timu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha moto katika soko la kimataifa la Kariakoo ili kubaini nini kimesababisha au nani kasababisha moto huo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara na wakazi wa eneo la Kariakoo baada ya kukagua hatua zinazoendela kuchukuliwa kudhibiti moto huo, Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa kamati iliyoundwa ambayo itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa huo itajumuisha Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo itawakilishwa na Mkurugenzi wa Maafa.

Vingine ni Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikujumuisha Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Zimamoto pamoja na Taasisi ya Kupambana na Rushwa. 

Pia Waziri Mkuu alizitaja Wakala wa Majengo, Shirika la Umeme (TANESCO), Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)

"Endapo itagundulika kama kuna mtu alihusika kwa namna moja au nyingine, hatua kali za kisheria zitachukuliwa moja kwa moja, kitendo cha kuungua kwa soko hili la miaka chungu mzima lazima kuwe na uchunguzi wa kina, kwanini leo lishike moto"