Wakala wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA), wilayani Mbozi mkoani Songwe, umesema ujenzi wa mradi mkubwa wa barabara ya Ilolo, Ndolezi yalipo makumbusho ya Kimondo cha Mbozi, inayojengwa wa kiwango cha lami, imefikia asilimia sitini huku ikitarajiwa kuwekewa taa arobaini katika maeneo yenye makazi ya watu.
Kaimu Meneja TARURA, Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Robert Mwakitalima, ameiambia ITV kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi, zitakazochagizwa na uwepo wa Makumbusho ya Kimondo cha Mbozi inapopita barabara hiyo, ambapo pia itakuwa na uwezo wa kupitisha magari makubwa yenye uzito wa tani arobaini.
Mradi wa barabara hiyo itakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni sita, ulianza kutekelezwa mwezi April 2023, na unatarajiwa kukamilika mwezi wa nne mwaka 2024.