Back to top

BILIONI 1.2 ZAPATIKANA KWENYE MAUZO YA MNADA WA VITO MANYARA

16 December 2024
Share

Kiasi cha shilingi Bilioni 1.2 kimepatikana kwenye mnada wa kwanza wa mauzo ya madini ya vito uliofanyika katika mji wa Mererani-Simanjiro Mkoa wa Manyara. 

Kiasi hicho cha fedha kimepatikana baada ya mauzo ya Gramu 163,093.32 zilizouzwa katika mnada huo ambao umeendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania(TMX) ikishirikiana na Wizara ya fedha na Wizara ya Madini.

Mnada huo ambao umezinduliwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde, ni sehemu ya muendelezo wa mauzo ya madini hayo ambayo itaendelea kufanyika kwa njia ya kielektroniki ili kutoa nafasi ya ushiriki kwa wadau wengi zaidi.

Goodluck Luhanjo Afisa Tehama kutoka TMX, amesema kuwa uwazi uliopo katika minada hiyo, unazidi kujenga imani ya Serikali kwa wauzaji na wanunuzi hali ambayo utazidi kuleta ushindani katika minada inayofuata.

Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mnada huo Disemba 13, 2024 Waziri wa Madini Anthony Mavunde, alieleza namna ambavyo sekta ya madini ya vito inakuwa kwa kasi duniani.

Mavunde amesisitiza kuwa uendeshaji wa minada hiyo kielektroniki chini ya usimamizi wa soko la bidhaa Tanzania utazidisha uwazi na ushindani sokoni.

"Urejeshaji wa minada ya madini haya ya vito, ni dhamira ya serikali inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kusimamia sekta ya madini kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali hii"Amesema Mavunde

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha minada hiyo ya madini ya vito ambayo itaendeshwa kwa uwazi kupitia mfumo wa kielektroniki, uliojengwa na Soko la bidhaa Tanzania TMX kwa ushirikiano wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini.