Serikali imesema katika mwaka wa fedha 2021/22, imepanga kutumia shilingi bilioni 312.09 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Elimu ya Msingi Bila Malipo ambazo ni ongezeko la shilingi bilioni 13.96 ikilinganishwa na shilingi bilioni 298.13 zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2020/21.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.David Silinde amesema hayo bungeni wakati akijibu swali la mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe.Hassan Mtenga aliyetaka kujua mkakati wa serikali wa kuongeza ruzuku katika mpango wa utoaji bure Elimu ya Sekondari na Msingi.
Mh.Silinde amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Elimu msingi bila Malipo kwa kadri ya mahitaji na upatikanaji wa fedha na kwamba hadi sasa imetoa shilingi trilioni 1.26 kwa ajili ya Elimu msingi bila malipo.
Akijibu swali la Mbunge wa Mtama Mhe.Nape Nnauye kuhusu umuhimu wa kuhusisha elimu ya kidato cha tano na sita kwenye elimu msingi ili nayo itolewe bila malipo, Mhe.Silinde amesema ni suala la kisera na serikali italiangalia, kuona namna ya kulifanyia kazi kulingana na mazingira.