Back to top

BITEKO AWAHIMIZA WATANZANIA KULIOMBEA TAIFA

17 February 2025
Share

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiombea nchi pamoja na Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“ Tuendelee kuliombea kanisa, tuendelee kuiombea nchi yetu na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae kwa kweli anafanya kazi nzuri na sisi tunaofanya kazi karibu naye tunaona,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akishiriki ibada katika Kanisa la Africa Inland Church Chang’ombe jijini Dar es salaam.

Amewahimiza Watanzania kudumisha upendo na amani nyakati zote hususan kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, ili uchaguzi huo usiwe sababu ya kuligawa Taifa kutokana na tofauti ya mitazamo.
 
Amesisitiza “ Mungu ametupa bahati ya kuwa na nchi yenye amani, sisi tuilinde kwa wivu mkubwa kwa kuwa amani ikiondoka gharama yake ni kubwa. Tuziombee  pia nchi jirani zenye matatizo kwa vile tatizo la jirani linaweza kuwa tatizo lako wakati wowote ule, mfano mnakumbuka janga la covid 19 lilivyotuathiri dunia nzima.”

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha mipango na sera mbalimbali  ili kuendana na mahitaji ya dunia, ametolea mfano mabadiliko yaliyofanyika katika Sera ya Elimu.

“ Tunatengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo tulizunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ya watu katika makundi mbalimbali ili tuweze kupata Tanzania tunayoitaka miaka 25 ijayo,” amebainisha Dkt. Biteko.

Akihuburi wakati wa ibada hiyo, Mchungaji Dkt. Joseph Mayala Mitinje amewaasa waumini wa Kanisa hilo kukumbuka kufanya maombi na kusema kuwa ibada hiyo ilikuwa maalum kwa ajili kuiombea Serikali pamoja na mahitaji mbalimbali.

“Ili umtumie Mungu vizuri una mahitaji ya kila eneo hivyo asubuhi ya leo tunaombea mahitaji yetu kwa Bwana,” amesema Mchungaji Mitinje.

Aidha, amendelea kwa kuliombea Taifa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali  katika kutekeleza majukumu yo huku akimuomba Mungu  akibariki Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani, umoja na mshikamano.

Naye, Mchungaji Andrew Chad kutoka nchini Uingereza akihubiri katika ibada hiyo amesema makanisa ya Uingereza na Tanzania yamekuwa na ushirikiano wa karibu na hivyo imeendelea kumpa fursa ya kuhubiri injili nchini.

Ambapo ameeleza kuwa  alipokuja nchini  alianza kuhubiri injili katika Kanisa la AICT Mpanda mkoani Rukwa kwa muda wa miaka nane. Baadaye yeye na wenzake  walianzisha makanisa mengi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mkoani Tanga ambapo alihudumu kwa muda wa miaka sita.

“ Tulipata wito kwenda mkoani Tanga kuhubiri injili kwa upande wa watu wa kabila la Wadigo na kuwafundisha watu wanampenda Mungu,” amesema Mchungaji Chad.

Ameongeza kuwa Mungu anaweza kumtumia binadamu yeyote kwa utukufu wake, sambamba na kuwaasa wakristu kuishi kwa upendo na kuwa wakarimu kwa watu mbalimbali.