
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, imeteketeza ekari 336 za mashamba ya bangi yaliyokuwa ndani ya hifadhi ya Ikome wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma yakiwa yamechanganywa na mazao mengine halali ili kuficha shughuli hiyo haramu, Aidha, katika operesheni hiyo, kilo 148 za mirungi zilkamatwa.
Akizungumza wilayani Kondoa, wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo ameeleza kuwa, operesheni hiyo ni hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya. "Hii ni operesheni kubwa ya kwanza kufanyika mkoani Dodoma, ikionyesha wazi kuwa kilimo cha bangi kimeanza kuenea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huu. Tutaendelea kuchukua hatua kali kuhakikisha kuwa uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya vinadhibitiwa kwa nguvu zote," alisema Lyimo.
Pamoja na operesheni hiyo ameongeza kuwa, katika kipindi cha Januari hadi Februari 2025, DCEA kupitia ofisi zake za kanda, imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 790.528 za aina mbalimbali ya dawa za kulevya katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam. Aidha, mashamba mengi ya bangi yaliteketezwa, huku watuhumiwa 114 wakikamatwa kwa kujihusisha na biashara hii haramu.
Katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam, watuhumiwa watatu walikamatwa wakiwa na kilogramu 32.16 za bangi aina ya skanka. Pia, watuhumiwa wanne walikamatwa wakiwa na kilogramu 5.1 za heroin pamoja na lita tano za kemikali aina ya Caffeine Anhydrous Pure, ambayo hutumiwa kuongeza wingi wa dawa za kulevya.
Mkoani Arusha, jumla ya kilogramu 98.55 za bangi, kilogramu 162.111 za mirungi, gramu 301 za heroin na gramu 195 za dawa aina ya methadone, pembe moja ya ndovu na risasi 11 za moto vilikamatwa. Katika tukio lingine mkoani humo, mtu mmoja alikamatwa akiwa ameotesha miche ya bangi ndani ya nyumba yake kwa kutumia glasi za plastiki (disposable).
“Matokeo haya yanathibitisha kuwa uhalifu wa dawa za kulevya mara nyingi huambatana na uhalifu mwingine, ikiwemo biashara haramu ya silaha na ujangili wa wanyamapori. Pia kuwepo kwa ongezeko la uchakachuaji wa dawa za kulevya kwa kuchanganya kemikali na vitu vingine ili kuongeza wingi wa dawa hizo kunaongeza athari za kiafya kwa mtumiaji” amesisitiza Lyimo.