Back to top

Dereva wa basi la shule ya Nyamuge afariki.

23 August 2018
Share

Dereva wa basi la shule ya Nyamuge iliyopo Nyasaka, wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, Bwana ALBERT JORAM amefariki papo hapo, na wanafunzi watatu wa shule hiyo wakijeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea eneo la Nyamhongolo karibu na viwanja vya Maonesho ya Nane Nane.

Katika ajali hiyo dereva wa basi la shule ya msingi binafsi Kivulini iliyopo Kisesa Wilayani Magu, Bwana KULWA CHARLES amevunjika mguu wa kulia na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Wanafunzi wa shule ya msingi Nyamuge waliojeruhiwa wametajwa kuwa ni DEVOTA BENNY wa Darasa la Tano ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa Bugando baada ya kuvunjika miguu yote miwili.

Wanafunzi wengine wa shule hiyo waliolazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure ni pamoja na DANIELA EDMUND ambaye amepata majeraha kichwani na REBECA FRANCIS.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Mkuu wa Idara ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Dakta SHAHZMAH SULEIMAN amethibitisha kupokea mwili wa dereva wa gari iliyogongwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Bwana AHMED MSANGI amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.