Serikali imewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa yasiyo sahihi ya vidonge vya kuzuia mimba maarufu kama P2 ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza pale dawa hizo zinapotumika bila utaratibu ikiwemo mvurugiko wa hedhi.
.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Medard Ntara aliyeuliza Je, kuna mpango gani wa kuruhusu Sayana Press kama njia ya Uzazi wa Mpango badala ya kutumia P2 bila utaratibu.
.
Dkt.Mollel amefafanua kuwa P2 ni njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango ambayo hutumika kuzuia mimba kwa mwanamke aliyefanya tendo la kujamiiana bila kinga kwa mfano aliyebakwa au ametumia kondomu ikapasuka na anadhani anaweza kupata mimba asiyoitarajia, na Sayana Press ni njia ya kuzuia kupata ujauzito kwa muda mrefu, hivyo matumizi ya kuzuia mimba kwa Sayana Press na P2 ni tofauti.
.
Aidha, Dkt. Mollel ameongeza kuwa Sayana Press imesajiliwa na TMDA na inapatikana kwenye vituo binafsi vya kutolea huduma za afya kwa wateja wanaohitaji.