Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, amejikuta katika hali ngumu jana wakati alipokuwa akihojiwa ndani ya Seneti katika kesi ya kuondolewa madarakani, aliyowasilisha kwa bunge dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Gachagua kupitia mawakili wake wazoefu wanaoongozwa na Wakili Paul Mwite, wanapambana kuhakikisha haondolewi mamlakani baada ya Bunge la taifa mnamo Oktoba 8 kupiga kura kuidhinisha kutimuliwa kwake.
Mutuse alipata kibarua kigumu kujibu maswali makali ya wakili wa Gachagua Elisha Ongoya, ambaye aliupinga ushahidi wake mkuu dhidi ya Gachagua.
Miongoni mwa tuhuma ambazo wanasheria wa Gachagua walitaka kuzifuta ni pamoja na kuihujumu serikali kwa kupinga hadharani sera zake za kuwahamisha wafanyabiashara kutoka soko la wakulima na kuwapeleka katika eneo jipya katika Barabara ya Outering na ubomoaji wa majengo katika maeneo ya mabondeni.
Timu ya Gachagua ilitumia kanda za video kuwadhihirishia Maseneta kuwa alitoa matamshi akiiomba serikali kuwatendea raia utu na zile zilizoonyesha kuwa baadhi ya kauli zilizotajwa kuchochea ukabila zimekuwa zikitumiwa tangu awali pia na Rais William Ruto.
Mawakili wa Gachagua walitoa video ambapo alitoa matamshi akiiomba serikali kuwatendea raia utu kwa kuzingatia ahadi zake za kabla ya kampeni.
“Naibu Rais anasema ‘Tusiwe na vita na Wananchi.’ Je, unaona jambo lolote la kuudhi katika taarifa hiyo?” Ongoya alimuuliza, Mutuse aliyejibu, hapana.
Wakati mmoja kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea wakili wa Gachagua, alicheza kanda ya video ambapo Rais Ruto alionekana kwenye mkutano akiwaambia wananchi wa eneo la Mlima Kenya kuwa wana 'share' (hisa) katika serikali- kauli ambayo bunge linasema imekuwa ikitumiwa na Gachagua na inachochea ukabila. Gachagua alisema alijifunza kutumia kauli hiyo kutoka kwa Rais Ruto.
Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa na seneti leo asubuhi.