Mtuhumiwa mkuu wa mauji ya kimbari ya Rwanda aliyekuwa mafichoni nchini Ufaransa kabla ya kukamatwa juma moja lililopita Félicien Kabuga, anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Paris, Ufaransa.
Félicien Kabuga aliyekuwa mfadhili huyo wa mauaji hayo yaliyotokea mwaka 1994 jana alifikishwa mbele ya Mwendesha Mashitaka mkuu jijini Paris.
Mahakama ya Paris itaamua iwapo itamkabidhi Kabuga katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa ambayo imechukua nafasi ya ile iliyokuwa inashughulikia kesi za Kimbari nchini Rwanda iliyokuwa jijini Arusha.
Majaji watakuwa na siku kumi na tano za kuamua juu ya uhalali wa hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama Maalum ya Kimataifa ambayo ina majukumu ya kukamilisha kazi ya mahakama iliyokuwa inashughulikia kesi za Kimbari nchini Rwanda iliyokuwa jijini Arusha.