Baraza la Michezo ya Majeshi kwa Nchi za Afrika ( Organization of Military Sports in Africa- OSMA), limemtunukia nishani ya utendaji bora (OSMA ORDER OF MERIT) iitwayo OFFICER , Kanali Joseph Bakari ( JWTZ).
Kanali Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani ( CISM ), Mratibu wa Bara la Afrika ( African Liaison Officer), na Mwakilishi wa Tanzania katika Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani ( CISM) ametunukiwa Nishani hiyo, kutokana na mchango na juhudi zake katika kueneza diplomasia ya michezo ya Majeshi kwa kutumia michezo na mafunzo ya utimamu wa mwili baina ya nchi wanachama kama njia ya kueneza amani duniani badala ya vita.
Nishani hiyo alivishwa na Rais wa Baraza hilo Meja Jenerali Maikano Abdullahi ( Nigeria), wakati wa sherehe za ufungaji wa Mkutano Mkuu wa Mwaka Muhula wa 8 wa Baraza hilo, tarehe 2 Machi 2O24 jijini Abuja Nigeria.
Akizungumzia utendaji wa Kanali Bakari, kabla ya kumvisha nishani hiyo, Meja Jenerali Maikano alisema kuwa, Bodi ya Wakurugenzi ya OSMA imeamua kumtunukia nishani hiyo ya juu, Kanali Bakari kutokana na kukidhi sifa na vigezo vilivyopo hasa utendaji wake bora.
Pamoja na Kanali Bakari wengine waliotunukiwa Nishani ni Brigedia Abdulraheem Bello ( Nigeria).
OSMA ni baraza la Michezo ya Majeshi kwa nchi za Afrika lenye wanachama 54, lililoanzishwa mwaka 1994 lenye lengo kuu la kuratibu ushiriki wa nchi za Afrika katika kutekeleza dhamira ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani ya kutumia michezo ya Majeshi na mafunzo ya utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani badala ya vita.