Ndege aina ya Korongo, wanaothaminiwa sana , wameripotiwa kupungua katika Wilaya ya Lwengo nchini Uganda baada ya waganga wa kienyeji kuwaambia wateja wao kuwa ndege hao ni wazuri kwa kafara kwa madai kuwa wana vitu vinavyosaidia kutatua masuala ya familia na kuokoa ndoa.
Afisa wa Mazingira wa Wilaya ya Lwengo,Bi Mary Jude Namulema, alisema uchunguzi wao wa hivi majuzi ulifichua kuwa waganga hao wa kienyeji huwahadaa wateja wao kwa kuamini kuwa mayai ya korongo na vifaranga vyao yanaweza kusaidia wanandoa kukaa kwa amani kama korongo wanavyoishi wawili wawili, jambo ambalo anasema limesababisha ndege wengi kuuawa, haswa wakati wa kuzaliana Novemba, Desemba na Januari.
Bi Namulema, hata hivyo, alitoa wito kwa waganga wa kienyeji na umma kuacha tabia hii kwa sababu itasababisha kutoweka kwa ndege huyo.