Ongezeko la mimba za utotoni katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, limetajwa kuchangia ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na hata kusababisha vifo, hali iliyopelekea serikali ya Wilaya kuweka mikakati madhubuti ya kukabliliana na matukio hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga mkuu wa Wilaya ya Masasi,Dr.Salum Gembe katika kilele cha siku ya vijana, ambapo amesema matukio ya kujamiiana katika umri mdogo ni chanzo kingine cha ukatili wa kijinsia.
Amesema katika Wilaya hiyo ongezeko la mabinti wanaopata mimba chini ya umri wa miaka 20 ni kubwa hivyo kama Wilaya imeendelea kutoa elimu ili kupunguza kiwango hicho ambacho pia ni hatarishi katika maswala ya uzazi.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Afya Yangu, unashughulika na vijana, Aboubakar Rehani amesema baadhi ya mila na desturi zinachangia kwa kiwango kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa vijana na hivyo baadhi kujikuta wakipata ujauzito wangali watoto.
Hata hivyo amesema mradi huo umekuwa ukitoa elimu kwa vijana wa Wilaya ya Masasi ikiwa ni pamoja na kupima afya zao mara kwa mara, na kuwaasa kutofanya tendo la ndoa wakiwa na umri mdogo kwani linaweza kukatisha ndoto zao.