Back to top

Mkuu wa mkoa atoa ahadi ya kukinusuru kiwanda cha Sukari cha Kagera

19 September 2018
Share

Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ameahidi kungoza jitihada  za kukomesha vitendo vya wafanyabiashara vya kuingiza Sukari toka nje ya nchi kwa njia ya magendo kupitia mpaka wa  mkoa huo na nchi  za Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya ili kukinusuru kiwanda hicho.

Anatoa kauli hiyo wakati wa  ziara yake kukitembelea kiwanda hicho na kupata fursa ya kujionea mashamba ya miwa na kiasi kikubwa cha sukari iliyorundikana kwenye maghala  huku meneja  mkuu wa kiwanda hicho Ashwin Rana akisema  lengo la uzalishaji katika msimu huu ni tani zaidi ya 85,000 na kubainisha kuwa hadi sasa tani ya 25,000  zimeishazalishwa na hazina soko.

Aidha, Brigedia Jenerali Gaguti ametoa ushauri kwa uongozi wa kiwanda hicho kuongeza idadi ya mawakala watakaopewa jukumu la kusambaza sukari katika maeneo mbalimbali yaliyoko mkoani Kagera na mikoa ya jirani ili sukari inayozalishwa na kiwanda hicho isambazwe katika maeneo mengi.

Naye mhandisi Nestory Rwechungula ambaye ni meneja wa kiwanda amemweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa kiwanda hicho hivi karibuni kitafunga  mtambo utakaozalisha umeme wa megawati 23 ambao sehemu yake itaunganishwa kwenye mtandao wa umeme wa gridi ya taifa.