Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, mlinzi wa Shule ya Sekondari Scolastica, Hamisi Chacha baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi wa Kidato cha pili katika shule hiyo, Humphrey Makundi.
Hukumu hiyo imesomwa leo na Jaji Frimini Matogolo baada ya kusikiliza kesi hiyo ya mauji ya kukusudia namba 48 ya mwaka 2018 ambayo ilianza kusikilizwa tangu Aprili mwaka huu.
Jaji Matogolo amesema,Hamisi Chacha ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ametiwa hatiani baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na mashahidi 18 pamoja na mshitakiwa kukiri kutenda kosa la mauaji mbele ya mlinzi wa amani kwa kumshambulia mwanafunzi huyo kwa panga.
Katika keshi hiyo mshitakiwa wa pili Edward shayo ambaye ni mmiliki wa shule ya Sekondari Scolastica na mshitakiwa wa tatu, Labani Nabiswa ambaye ni mwalimu wa nidhamu wamehukumiwa kifungo cha miaka minne jela baada ya kukutwa na hatia ya kushirikiana kwenda kuutupa mwili wa mwanafunzi huyo kwenye korongo la Mto Ghona, mita mia 300 kutoka shuleni hapo ili kupoteza ushahidi.