Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ameliagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuhakikisha linatatua kero ya mawasiliano inayowakabili wananchi wa Vijiji vya Mlengu na Kigala vilivyopo katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kukamilisha ujenzi wa minara itakayosaidia kutoa huduma ya mawasiliano ya simu kwa wananchi.
Naibu Waziri ametoa agizo hilo katika Kijiji cha Kigala wilayani Makete wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miundombinu mbalimbali ya watoa huduma za mawasiliano katika wilaya hiyo, ambapo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma za mawasiliano.
Kwa upande wake, Meneja wa TTCL Mkoa wa Iringa na Njombe, Chavala Matona amesema mradi huo ambao umefadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unalenga kutatua changamoto ya mawasiliano kijijini hapo na wameanza ujenzi wa mnara unaogharimu shilingi milioni 300 na kuwa vifaa vyake vyote vipo tayari .