Mahakama Kuu ya jimbo la Gauteng, Afrika Kusini, leo imetoa hukumu na kuamuru ndege ya Air Tanzania Airbus A220-300 iliyokuwa inashikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi.
Taarifa ya kuachiwa kwa ndege ya Tanzania imethibitishwa na Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk.Hassan Abbas ambaye ameichapisha taarifa hiyo kupitia kwenye mtandao wa Twitter huku akimalizia na maneno yasemayo "Tuna washukuru wote kwa uvumilivu wenu.
Kwa upande wake Naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki Dkt.Damas Ndumbaro ambaye alikuwa nchini Afrika Kusini kufuatilia mkasa huo wa kushikiliwa kwa ndege ya Tanzania, amesema serikali itatekeleza maelezo yote yaliyotolewa na mahakama na sasa ndege iko huru na itaendelea na shughuli zake za kila siku kulingana na taratibu za ratiba yake.
Na ndege hiyo Airbus A220-300 kwa sasa iko njiani ikirejea hapa nchini.