Back to top

PINDA AKABIDHI HUNDI YA MIL 45 KUTOKA CRDB KWA WAJASIRIAMALI MPIMBWE

12 September 2024
Share

Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amekabidhi hundi ya shilingi milioni 45 kwa vikundi vitatu vya wajasiriamali wa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi kutoka benki ya CRDB kuvijengea uwezo.

Mhe Pinda amekabidhi hundi hiyo, wakati akifungua semina ya siku moja ya kuvijengea uwezo vikundi vya wajasiriamali wanawake na vijana kunufaika na programu ya IMBEJU katika kata za halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoa wa Katavi iliyofanyika kata ya Majimoto.

IMBEJU ni fedha zinazotolewa na Benki ya CRDB bila riba kuwajengea uwezo wajasiliamali wadogo

Vikundi vilivyokabidhiwa kiasi hicho cha fedha ni Nguvumoja Kashishi, Imani Kashishi pamoja na kikundi kingine kitakachokidhi vigezo vya kuwezeshwa.

Akizungumza wakati wa kuzindua semina hiyo Mhe. Pinda amesema Ili kuendesha biashara kisasa ni lazima wajasiriamali wapate ushauri na mafunzo kutoka kwa wataalamu.

Ameeleza kuwa, taasisi za fedha kama CRDB ni miongoni mwa sehemu ya uhakika ambayo mjasiriamali anaweza kupata elimu ya fedha ya uhakika ili kufanikisha mipango ya biashara.

Amewataka wajasiriamali wa Mpimbwe kutumia fursa inayolingana na uwezo wao binafsi na siyo kusikia tu benki inatoa mitaji wezeshi na kulazimika hata kudanganya ili kukopa fedha pasipo mikakati makini ya kuzitumia.

Ameishukuru CRDB kupitia taaasisi yake ya CRDB Foundation kwa ubunifu wa kuwafikia wajasiriamali wadogo hata waliopo pembezoni kama vile Mpimbwe.

"Hii si jambo dogo kwa taasisis inayojiendesha kibiashara kutenga bajeti ya kuelimisha wananchi na kuwapa mitaji wrzeshi" alisema Mhe. Pinda

Washiriki wa semina hiyo ya siku moja wametoka kata za Mamba, Majimoto, Mwamapuli, Chamalendi, Mbede, Ikuba na  Usevya. Semina hiyo itaendelea katika kata za Kibaoni na Kasansa zitaendelea kesho.