
Mhandisi na wasimamizi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kigamboni jijini Dar es Salaam wameagizwa kufuata ramani mpya zilizotolewa na wizara katika ujenzi unaoendelea wa kituo hicho na kuacha kutumia ramani ya zamani.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali Mitaa TAMISEMI Mh.Josephat Kandege wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayoendelea katika wilaya ya Kigamboni ambapo amebaini ujenzi ulioanza katika kituo hicho kuwa unafuata ramani ya zamani huku akimtaka mhandisi kubadilisha mara moja na kutumia ramani mpya kama zilivyotolewa na wizara kwa vituo vya afya nchi nzima.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kigamboni Bi.Sara Msafiri amewataka watendaji wote kutoa ushirikiano wa ufanisi katika kutekeleza na kusimamia miradi yote kwa wakati huku mganga mkuu wa manispaa ya Kigamboni akisema ujenzi wa jengo hilo utasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa wengi ambapo watapata huduma kwa wakati katika kituo hicho.