Wakulima wa zao la Chai katika mkoa wa Kagera wameiomba serikali inusuru kilimo cha zao hilo katika ambacho kinaendelea kudorora kila kunapokucha kwa kuweka mazingira yatakayowahamasisha vijana katika mkoa huo kuchukua uamuzi wa kijihusisha na kilimo hicho ambacho huchangamkiwa zaidi na wazee.
Wakulima hao wametoa ombi hilo kwa serikali kwenye risala yao iliyosomwa na mwenyekiti wa wakulima wa zao hilo katika mkoa wa Kagera, Henry Rugakingira mbele ya katibu mkuu wa chama cha mapinduzi (CCM) taifa, Dkt.Bashiru Ally Kakulwa alipokutana na wakulima baada ya kutembelea kiwanda cha kusindika chai kilichoko mkoani humo.
Bw.Rugakingira amesema tatizo la bei ndilo linapelekea kudorora kwa kilimo cha zao hilo huku mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho Dkt. Aloyce Mgimba amesema mikakati yake ni kuhakikisha anawahamasisha wakulima waongeze uzalishaji wa chai.
kwa upande wake, Dkt. Bashiru Ally Kakulwa akizungumza na wakulima wa zao hilo pamoja na kumpongeza mwekezaji huyo amemuagiza asiwakatishe tamaa wakulima hao kwa kuchelewesha malipo hata kama ni kidogo huku mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti amesema mkoa huo umeshaanza kubuni mikakati mbalimbali ya kuboresha kilimo cha chai kwa kuwatafutia wakulima soko la uhakika.