Back to top

Shehena ya sampuli zaidi ya 800 za miamba ya madini zakamatwa Mwanza.

24 February 2019
Share

Kamati ya ulinzi na usalama mkoani Mwanza inalishikilia gari aina ya fuso lenye namba za usajili T.609 AGB, lililokua likisafirisha ndoo 226 zenye jumla ya sampuli za miamba ya madini 883 mali ya mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM ), zilizokuwa zikisafirishwa kutoka mkoani Geita kuelekea jijini Mwanza.

Gari hilo limekamatwa majira ya alfajiri na askari polisi waliokuwa doria baada ya kubaini kuwa shehena hiyo ya sampuli za madini iliyokuwa ikisafirishwa kwenda katika maabara ya kupima sampuli za madini ya SGS iliyopo jijini Mwanza, ilikuwa na upungufu wa vibali vinavyoruhusu mzigo kusafirishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, ameziagiza mamlaka husika mkoani humo kufuatilia na kuchunguza uhalali wa usafirshaji wa sampuli hizo pamoja na kuwataka watendaji wa serikali kufanya kazi kwa uadilifu.