Serikali ya Tanzania imeungana na nchi nyingine za afrika kwa kutangaza kurejesha na kuhifadhi zaidi ya hekta milioni tano na laki mbili za misitu ya asili ifikapo mwaka 2030 ili kuunga mkono juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na uharibifu wa misitu ya asili
Akiongea kwenye tukio hilo la kitaifa la kutangaza dhamira ya serikali ya Tanzania iliyofanyika katika misitu ya Kazimzumbwi Kisarawe mkoani Pwani, naibu waziri wa maliasili na utalii Mhe.Japhet Hasunga amesema kwa hatua hiyo Tanzania imeungana na nchi nyingine barani Afrika kuhifadhi jumla ya hekta milioni 100 ifikapo mwaka 2030 mpango ambao kwa Tanzania utasimamiwa na wakala wa huduma za misitu nchini TFS kwa kushirikiana na wadau wengine wa uhifadhi
Mapema taarifa ya mtendaji mkuu wa wakala wa huduma za misitu nchini TFS Profesa Dosantos Silayo imeeleza kuwa Tanzania inakuwa nchi ya 22 barani Afrika kutangaza dhamira hiyo ambapo mkurugenzi mkazi wa shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira WWF Dkt.Amani Ngusaru amesema WWF itakuwa mshirika mkubwa kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania katika uhifadhi huo na katika hafla hiyo WWF na TFS wakatiliana saini mkataba wa mkakati wa kuokoa na kuendeleza uhifadhi misitu ya Tanzania.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amesema serikali ya wamu ya tano inatambua umuhimu wa kuhifadhi misitu ikiwemo ya Pugu Kazimzumbwi na Ruvu Kusini na amewataka wavamizi wote kuondoka katika misitu hiyo mara moja ili kupisha uhifadhi endelevu wa misitu hiyo yenye umuhimu kitaifa na kimataifa.
Katika hafla hiyo iliyohudhuliwa na wadau mbalimbali wa uhifadhi wa ndani na nje ya nchi serikali imezindua mpango wa upandaji miti ya asili kwenye misitu hiyo ya Pugu Kazimzumbwi ambayo ilikuwa imeathiriwa na wavamizi na ongezeko la shughuli za binadamu.