Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Judith Kapinga, amesema serikali inania ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi, ambapo amesema tayari maeneo matano yameshabainishwa kwa ajili ya kupata nishati hiyo ya Jotoardhi ikiwemo Ruhoi, Natron, Mbozi, Songwe na Kiejo-Mbaka.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumzia uzalishaji umeme kwa kutumia Jotoardhi, Mhe. Kapinga amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na vyanzo vyenye uwezo kuzalisha Megawati 5,000 na kwamba tayari Rais ametoa shilingi bilioni 15.7, kwa ajili ya kununua mitambo ya uchorongaji wa maeneo, ambayo yamebainika kuwa na rasilimali ya jotoardhi.
Kuhusu Nishati Jadidifu amesema mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita, ni kuendeleza zaidi vyanzo vya nishati jadidifu, ili kupunguza utegemezi wa kiuchumi, kuongeza usalama wa nishati na kuleta uendelevu wa kinishati ambao unachangia kiasi kikubwa katika kulinda mazingira.