Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa dawa, chakula na vifaa vya kujihifadhi kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa kimbunga cha Idai kilichosababisha mafuriko yaliyozikumba nchi hizo tangu wiki iliyopita.
Msaada huo umekabidhiwa kwa Mabalozi wa nchi hizo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambako sehemu ya msaada huo kwenda nchi za Zimbabwe na Msumbiji unasafirishwa leo kwa kutumia ndege za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akizungumza wakati zoezi la kupakia msaada huo katika ndege ya Jeshi likiendelea Mhe. Prof. Kabudi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kutolewa kwa msaada huo sambamba na salamu za pole kwa Marais wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe pamoja na wananchi wa nchi hizo kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo.
“Kwa hivyo Mhe. Rais Magufuli baada ya kupata taarifa hizi na kuzungumza na Marais wenzake wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, Tanzania imeona ni vyema kutokana na undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze kuwapelekea msaada angalau kidogo wa dawa na chakula na pia kuwapa pole kwa maafa haya makubwa yaliyowapata” amesema Prof. Kabudi.
Amebainisha kuwa kati ya msaada huo malori 7 yenye shehena ya tani 200 za mahindi yanaondoka leo kutoka Mbeya kwenda nchini Malawi ambako taarifa zinaonesha watu 122 wamepoteza maisha na zaidi ya 1,000 wamekosa mahali pa kuishi, tani 7 za mchele, dawa na vifaa vya kujihifadhi zinaondoka Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya Jeshi kwenda Msumbiji ambako taarifa zinasema watu 221 wamefariki dunia na tani nyingine 7 za mchele, chakula na vifaa vya kujifadhi zinaondoka Dar es Salaam kwa ndege ya Jeshi kwenda nchini Zimbabwe ambako watu 98 wamefariki dunia.
Kwa upande wake Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imetoa tani 24 za dawa ambapo kila nchi itapatiwa tani 8 zinazojumuisha dawa za kuzuia maambukizi ya magonjwa (antibiotics), dawa za magonjwa ya tumbo, dawa za kutuliza maumivu, dripu, shuka, blanketi, magodoro na vyandarua.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya nchi yake Balozi wa Msumbiji hapa nchini Mhe. Monica Mussa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali ya Tanzania kwa msaada huo ambao amesema utasaidia kunusuru maisha ya watu wengi ambao hawana chakula, wanahitaji dawa na wanahitaji malazi.
Nae Balozi wa Malawi hapa nchini Mhe. Glad Chembe Munthali amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali, na kueleza kuwa msaada huo wa haraka umedhihirisha udugu, ujirani na umoja wa dhati uliopo kati ya Tanzania na Malawi.
Kaimu Balozi wa Zimbabwe hapa nchini Bw. Martin Chavenika pamoja na kutoa shukrani zake za dhati amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli na Serikali kwa ujumla kuwa msaada huo utawafikia walengwa.
Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa Kamandi ya Jeshi la Anga Brig. Jen. Francis Shirima amesema Jeshi litahakikisha msaada wote uliotolewa unafika leo kwa nchi hizo na kukabidhiwa kwa wahusika.