
Ujenzi wa kiwanda kipya cha kutengeneza dawa kiitwacho M- pharmaceutical Ltd, umezinduliwa eneo la Kerege,wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani kwa kuwekewa jiwe la msingi na Waziri wa Afya , Maendeleo ya jamii,Jinsia,wazee na watoto Mhe.Ummy Mwalimu.
Kiwanda hicho kinachojengwa kwa ubia Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi na Mwekezaji kutoka India kitagharimu dola za kimarekani milioni 55 sawa na shilingi bilioni 55 za Tanzania.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Dr Mengi kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais John Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya kisasa ya Taaluma na Tiba Muhimbili Mlonganzila.
Waziri Ummy Mwalimu pia amemhimiza Dr Mengi na mbia mwenzake kuharakisha ujenzi wake na kumhakikishia kuwa bidhaa zitakazozalishwa zitapata soko kubwa hapa nchini na nchi za ukanda huu, na kunufaika na upendeleo maalum wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi amesema katika awamu ya kwanza kiwanda hicho kitazalisha chupa milioni 30 kwa mwaka za aina mbalimbali za maji ya dripu zinazotumiwa wakati wa matibabu ya dharura nyakati za ajali, upasuaji,homa kali,na magonjwa ya mlipuko, zinazokidhi vigezo vya kimataifa.
Amesema kipaumbele cha ajira kitatolewa kwa wananchi wa Bagamoyo, na kusisitiza kuwa umihimu wa Watanzania kujiamini katika kujiletea maendeleo.
Mapema Waziri wa Viwanda na Uwekezaji dk charles Mwijage na mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikiro amewataka viongozi wasiwakwamishe wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika maeneo yao, na kwamba serikali itashughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji, umeme wa uhakika na gesi asilia katika eneo hilo.
Uwekaji jiwe la msingi ulishuhudiwa na wananchi wa Kerege, Balozi wa Ufaransa Frederic Clavier, balozi wa China Wang Ke, Mbunge wa Bagamoyo Dr Shukuru Kawambwa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno na viongozi mbalimbali mbalimbali wa serikali na CCM wa mkoa na wilaya ya Bagamoyo.