
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof.Riziki Shemdoe, amewahimiza wadau wa Sekta ya Uvuvi kujikita katika ufugaji wa viumbe maji, ili kusaidia kukuza mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa kutoka asilimia 1.7 walau kufika mpaka asilimia 5 ifikapo mwaka 2025.
Prof.Shemdoe ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa Ukuzaji Viumbe maji kilichofanyika Jijini Dodoma Oktoba 31, 2023.
Amesema kuwa hivi sasa wanaandaa kanuni zitakazosaidia kuwa na usimamizi madhubuti wa tasnia ya uvuvi kwa lengo la kuimarisha ukuzaji wa viumbe maji ili kuchangia vyema katika Pato la Taifa.
"Tunaandaa kanuni kwa ajili ya ufugaji viumbe maji , kwenye ufugaji wa samaki na mavuvi ya samaki ili kuona namna tutaweza ndani ya miaka hii miwili kuchangia asilimia 5 kwenye pato la taifa,"Amesema Prof.Shemdoe
Ameongeza kuwa kanuni hizo zitakwenda kuboresha namna tasnia ya ukuzaji viumbe maji inasimamiwa na kuwezesha kile kinachozalishwa kiweze kufika kwenye masoko makubwa ya kikanda na kimataifa
Naye Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Bi.Agness Meena, amesema kupitia kikao hicho wadau watapata fursa ya kubainisha changamoto zinazoikabili tasnia ya ukuzaji viumbe maji na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo na kuongeza uelewa kuhusu usimamizi shirikishi na kuwa na tasnia endelevu.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala amesema tasnia ya ukuzaji viumbe maji itakuja kuwa na mchango mkubwa sana kwenye Sekta ya Uvuvi kwa vile bado ni ndogo na inakuwa kwa haraka.
"Tanzania tuna bahati ya kuwa na rasilimali nyingi za maji kwa maana ya maziwa, mabwawa makubwa, maji ya chini ya ardhi, ambayo yanaweza kuchimbwa na sehemu yoyote ikafanyika ufugaji wa samakikatika mabwawana tukiweza kufanya hivi tunaweza tukaongeza fursa zaidi za ajira, na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na jamii kwa ujumla"Amesema Dkt.Madala
Kikao hicho, kimefanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Shirika la Chakula na kilimo Duniani (FAO) Tamisemi pamoja na wafugaji wa samaki, lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu changamoto zilizopo na kubaini mikakati ya kuzitatua.