Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla ametangaza kiama kwa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini na kusema kuanzia sasa yeyote atakayekamatwa na mifugo yake itataifishwa kwa mujibu wa sheria.
Dkt.Kigwangalla ametoa tamko hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lyazumbi kinachopakana pori la akiba la Lwafi lililopo wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo.
Amesema Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, Kifungu cha 111 kinaruhusu kutaifisha mifugo na mali itakayokamatwa hifadhini.
Amesema kwa kipindi cha miezi tisa tangu ateuliwe kuiongoza wizara hiyo amekuwa akitoa msamaha kwa wnanchi wanaokamatwa na mifugo hifadhini jambo ambalo kwa sasa hatofanya tena kwakuwa kama ni elimu imeshatolewa vya kutosha.
"Maeneo ya hifadhi sio shamba la bibi lisilokuwa na mwenyewe, ni lazima watu waheshimu sheria za uhifadhi, nawahakikishia tukiwakuta kwenye maeneo ya hifadhi, tutawakamata na kutaifisha mifugo yenu, ahkutakuwa na huruma wala msalia mtume" alisisitiza Dk. Kigwangalla.
Wakati huo huo Dkt.Kigwangalla ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuwasilisha ahadi iliyotolewa na Waziri aliyemtangulia ya shilingi milioni 3 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Kizi. Pia ameiagiza mamlaka hiyo kuchangia mabati kwa ajili ya darasa moja katika kijiji hicho ili wananchi wanufaike na faida inayopatikana kwenye uhifadhi.