Serikali imeliambia bunge kuwa wazee waliopata ulemavu kutokana na vita vya Kagera, wapatao 272 bado wanalipwa pensheni ya ulemavu .
Naibu waziri wa mambo ya ndani Mh.Jumanne Sagini, amewataka wale ambao hawapo katika mfumo wa malipo hayo wajitokeze, ili waweze kuingizwa na kunufaika na malipo hayo ya pensheni.
Amesema mara baada ya vita hivyo wengi walioshiriki walipatiwa ajira, katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, polisi na magereza kwa wale waliokutwa na sifa za kuajiriwa na vyombo hivyo.
Naye Spika wa Bunge Mhe.Tulia Ackson, amemuagiza Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Ndani kumwambia waziri wake, waangalie jinsi ya kuendelea kuwahudumia wazee hao vizuri kutokana na mchango wao waliotoa kwa taifa.
Naibu Waziri Sagini, alikuwa akijibu swali lililoelekezwa kwa Serikali kuhusiana na jinsi ambavyo Serikali, inawahudumia wazee waliopigana vita vya Kagera.