Zaidi ya Wanafunzi wa kike 280 wanaotoka katika familia duni, wamepatiwa sare na vifaa vya shule vyenye thamani ya shilingi milioni 60 na Taasisi ya Haki Elimu, ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao ya sekondari bila changamoto.
Mkurugenzi Mtendaji Haki Elimu, Dkt.John Kalage, amesema Haki Elimu imeweza kutekeleza kazi mbalimbali ikiwa ni uanzishwaji wa vilabu vya kijinsia shuleni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wavulana na wasichana, kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia na haki za watoto ikiwa ni pamoja na kutambua dhana na aina ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na namna ya kukabiliana navyo.
Dkt.Kalage ameongeza kuwa mradi huu wa miaka mitatu unafadhiliwa na serikali ya Kanada na unatekelezwa katika jumla ya shule 67 (34 Msingi na 33 Sekondari) katika Wilaya 12 za Tanzania bara ambazo ni pamoja na Masasi, Kilwa, Mkuranga, Tunduru, Arusha, Babati, Bariadi, Tabora, Ukerewe, Serengeti, Geita na Sumbawanga lengo likiwa ni kupunguza mdondoko wa wasichana kwa kuhakikisha kuwa wasichana wanabaki shuleni na wanahitimu masomo yao katika mazingira rafiki na salama
Aidha ugawaji wa sare na vifaa vya shule kitaifa katika shule ya sekondari Dundani iliyopo Wilaya ya Mkuranga, ambayo ni shule mojawapo ya mradi, zoezi la ugawaji wa vifaa hivi limeongozwa na Mkuu wa Mahusiano ya Maendeelo wa Ubalozi wa Kanada.