Back to top

WATUMISHI WA UMMA JITOKEZENI MKAPIGE KURA – SIMBACHAWENE

26 November 2024
Share

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewasisitiza Watumishi wa Umma na Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika kesho Novemba 27, 2024 Tanzania Bara.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo Ofisini kwake katika Mji wa Serikali, Mtumba, Jijini Dodoma.

Mhe. Simbachawene amesema, zoezi la kesho ni la kihistoria katika nchi yetu hivyo kila Mtanzania mwenye sifa wakiwemo Watumishi wa Umma wote ni muhimu wakashiriki katika kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.

“Kwa kuwa zoezi hili ni la kikatiba, nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ninatoa rai kwa Watumishi wote wa Umma na wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu.” amesisitiza Mhe.Simbachawene

Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku ya kesho  kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa watumishi wote kwenda kupiga kura.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amewasisitiza Watumishi hao  kwenda kupiga kura bila kupuuza kwani ushiriki wao kwenye mambo muhimu ya kikatiba ni  kutekeleza majukumu ya kiutumishi.