Back to top

Wavuvi haramu nyumba ya Mungu wapewa wiki moja.

31 August 2018
Share

Wavuvi haramu wanaotumia nyavu aina ya makororo na nyingine za aina hiyo katika wilaya tatu zinazolizunguka bwawa la nyumba ya Mungu katika mikoa ya Kilimanjaro na Manyara wamepewa wiki moja wawe wamezisalimisha kwa hiari nyavu hizo katika ofisi za wenyeviti wa vijiji vinavyojihusisha na uvuvi kabla oparesheni maalum ya wavuvi haramu katika bwawa hilo haijaanza.

Mkurugenzi mkuu wa uvuvi katika wizara ya mifugo na uvuvi Bw.Magesa Bulayi ametoa agizo hilo alipozungumza na baadhi ya wavuvi wa kijiji cha Kagongo wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya kugundua kuwa uvuvi haramu bado unaendelea kwa kasi kubwa katika bwawa hilo.

Bw.Bulayi ameonya kuwa, baada ya wiki moja serikali haitakuwa na huruma na mvuvi ye yote na uvuvi haramu utabaki kuwa historia katika bwawa hilo na amewataka wavuvi hao sasa kuzingatia sheria na kanuni  bora za uvuvi kwa faida ya vizazi vijavyo.

Hata hivyo wavuvi katika kijiji hicho  wameiomba serikali iangalie namna bora ya kulifunga bwawa hilo kwa sababu   wamekuwa wakiathirika sana wakati linapofungwa kwa muda mrefu kwa kuwa tegemeo lao kubwa ni uvuvi.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw.William Mahuhu ameiomba serikali iwatafutie mitaji ya uvuvi na soko la uhakika wa samaki wanaovua katika bwawa hilo ili kujihakikishia maisha bora zaidi na familia zao.