Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), imewataka wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya Mifugo kupima ubora vya vyakula wanavyovizalisha, ili kujiridhisha kama vinakidhi ubora, unaotakiwa kwa lengo la kulinda afya za mifugo pamoja wa watumiaji wa mazao ya mifugo.
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo, amebainisha haya wakati akifanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo Mkoa wa Pwani (Kibaha, Mlandizi na Kisalawe), ili kujiridhisha kama taratibu zilizowekwa na wizara zinafuatwa ikiwemo uhuishaji na ukataji vibali vya uzalishaji na uuzaji wa vyakula vya mifugo Pamoja na kuhakiki ubora wa vyakula hivyo.
"Vyakula vyote vya mifugo vinavyozalishwa vinasimamiwa na sheria ya nyanda za malisho, ni lazima vyakula vyote viwe vimepimwa ili kujihakikishia viwango vilivyokubalika kwa matumizi ya Mifugo, mnatakiwa kujiridhisha kama chakula kimehakikiwa ubora na kinafaa kwa matumizi, tunapita kukagua pamoja na kutoa elimu. kwa wale tutakaowabaini wanavunja sharia, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, tusifanye kazi kwa mazoea, tunatakiwa kulinda afya za mifugo na walaji" Amesema Dkt. Makondo.
Kwa upande wake Mkaguzi wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kisalawe Mkoa wa Pwani Dkt. Kimboka Juma, amewataka wauzaji na wazalishaji wa vyakula vya Mifugo kuweka chapa kwenye mifuko ya vyakula, kuzingatia usafi wa mazingira ya kuuzia vyakula hivyo ili viendelee kubaki na ubora pamoja na kuajili wauzaji waliosomea vyakula vya Mifugo.
Meneja wa Kiwanda cha Animal Care Company ltd kilichopo Mlandizi mkoa wa Pwani Bw. Aijeno Ngogo, ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kuendelea kuwatembelea, kuwakagua na kuwapa ushauri wa vitu vinavyotakiwa kufuatwa na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ustawi wa Mifugo.