
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula, ameitaka Bodi ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kuwa wabunifu wa vyanzo vya mapato na kuweka msukumo kuhakikisha chuo hicho kinafanikiwa katika kutekeleza majukumu yake kisheria.
Aidha, ameitaka Bodi ya Chuo cha ARIMO kuhakikisha inapata taarifa kuhusiana na fedha za mkopo wa riba nafuu iliyopatiwa kwa ajili ya kazi za urasimishaji makazi holela ili mkopo huo uweze kurudishwa kwa wakati.
Dkt.Mabula amesema hayo wakati akizindua Bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) iliyofanyika chuoni hapo.
Bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro inaongozwa na Balozi Job Masima na imeanza kazi yake tarehe 1 Februari 2023 hadi tarehe 31 Januari 2026.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2022/2023 wizara ya Ardhi ilikipatia chuo mkopo usio na riba wa shilingi bilioni 1.273 zilizotumika katika utekelezaji wa mradi wa urasimishaji makazi katika mji wa Mbalizi halmashauri ya wilaya ya Mbeya.
Amesema Wizara yake imekuwa ikikisaidia Chuo katika masuala mbalimbali kama vile kukipatia msaada wa vifaa vya kisasa vya upimaji kwa ajili ya kufundisha na kutekeleza miradi mbalimbali.
"Wizara itaendelea kukisaidia Chuo cha ARIMO katika kuboresha miundombinu kupitia mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi, kupitia mradi huu ni vizuri ukatumika kama fursa ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo". Amesema Dkt.Mabula
Aliukumbusha uongozi wa Chuo cha ARIMO katika kuwatumia wanafunzi kwenye miradi ya kupanga na kupima ambapo alisema pamoja na utaratibu huo kuwa mzuri kutokana na kuongeza umahiri kwa wanafunzi lakini utekelezaji wake unapaswa kuzingatia ratiba ya wanafunzi wakati wa kwenda uwandani.