Back to top

SILAA ATANGAZA MAGEUZI MAKUBWA YA UPIMAJI NA RAMANI, ARDHI

09 May 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Jerry Silaa, amesema Mageuzi makubwa Sekta ya ardhi yanakuja baada ya kushuhudia utiaji saini kati ya Wizara yake na Mtaalamu Mshauri wa Mradi Mkubwa wa Kuimarisha na Kuboresha Miundombinu ya Upimaji na Ramani (LDI) wenye thamani takribani Bil. 150 za Kitanzania.

Waziri Silaa amebainisha kuwa Mradi huo utaongeza uwezo wa Wizara wa kuandaa ramani za msingi kwa nchi nzima ambazo licha ya kutumika katika kupanga matumizi ya Ardhi mijini na vijijini, pia zinahitajika kwa matumizi mengine mengi katika ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli, njia za mawasiliano, pia katika ulinzi na udhibiti wa maliasili, madini, ikiwemo mazingira.
 
Jerry Silaa amesema hayo wakati wa Hafla fupi ya utiaji Saini Mkataba wa kati ya Wizara na Mshauri Elekezi wa Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Upimaji na Ramani Bw.Kim, Ki Hwan atakayesimamia utekelezaji wa mradi huo hafla iliyofanyika Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

Mradi huu ukikamilika utawezesha huduma za ardhi za kuthamini, kupanga, na kupima kufanyika kwa haraka na kwa gharama nafuu sana, hivyo kufanikisha azma ya Serikali ya kupima kila kipande cha ardhi nchini.

Waziri Silaa ameongeza kuwa Mradi huu Mradi huu una vipengele vikuu vinne ambavyo ni Kuandaa ramani za msingi ambazo zitandaliwa katika Miji mikuu ya Mikoa 26 nchini yakiwemo Majiji na Manispaa zote na kuongeza kuwa mradi pia utaandaa ramani ya uwiano mdogo kwa nchi nzima.

Kipengele kingine ni kuweka vituo 30 vya upimaji vya kielektroniki ambapo Mradi utaweka Vituo vya CORS katika Miji Mikuu yote ya Mikoa, na kuongeza alama 357 za upimaji za kawaida  katika Miji hiyo, ambapo Vituo vya CORS vinaongeza kasi ya upimaji na kupunguza sana gharama ya vifaa na nguvukazi inayohitajika katika upimaji wa ardhi.
 
Aidha kiongozi huyo amebainisha kuwa mradi pia una kipingele cha Kujenga kanzidata ya taarifa za kijiografia   pamoja na mifumo ya kulinda na kusambaza taarifa hizo kwa watumiaji ili zipatikane kwa haraka, wakati wote na mahali popote.
 
Aidha mradi pia utawezesha Serikali Kununua vifaa vya vya kisasa vya upimaji ardhi na kuandaa ramani za msingi pamoja na Kujenga uwezo wa watanzania ili waweze kutekeleza mradi huu, na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za mradi hata baada ya kukamilika kwa mradi.

Wakati huohuo Katibu Mkuu Wizara vya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Eng. Anthony Sanga aliongeza kuwa Ramani ya msingi ya uwiano mdogo itaandaliwa kwa nchi nzima lakini pia Ramani za uwiano mkubwa zitaandaliwa kwa miji mikuu ya mikoa yote sambamba na uwekaji wa vituo vya upimaji vya kielektroniki na kuongeza alama za upimaji za kawaida.

Aidha Eng.Sanga amemtaka mtaalam huyo kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia makubaliano ya Mkataba huo ili thamani na matokeo ya mradi huo yaweze kuhakisi matamanio makubwa ya kufikia adhima ya kupima kila kipande cha ardhi hapa Nchini.