Back to top

TAWA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUWEKEZA NCHINI.

06 July 2024
Share

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imesema ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji, unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika Taasisi hiyo.

Afisa utalii kutoka TAWA Daud Tesha, amesema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika Taasisi hiyo, kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye Utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri, Uwindaji wa Kitalii na Ufugaji wa Wanyamapori.

Amesema TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha, kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo, ikiwemo Pori la Akiba Mpanga / Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10, ambayo hutoa burudani safi kwa watalii.

Tesha ameeleza hayo kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Kibiashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam, lengo ni kuhamasisha umma wa Watanzania, wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametumia  fursa hiyo kuwakaribisha wananchi Wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.